[Part 1 MABANDA] MAMBO 4 MUHIMU YA KUKUFANIKISHA KATIKA UFUGAJI KUKU.

Mambo 4 muhimu ya kukufanikisha katika ufugaji kuku. [Part 1]

Kuweza kufanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mfugaji  anahitaji muongozo mzuri na umakini katika MABANDA, CHAKULA BORA, UDHIBITI WA MAGONJWA na MASOKO.

Ni muhimu sana kwa mfugaji  kujifunza mambo kadhaa kabla ya kuingia kwenye ufugaji. Ni wajibu wetu [Sayuni Poultry Gosheni] kukushirikisha ufahamu huu, ili mfugaji binafsi awe muangalizi mkuu wa mradi wake; na awe na mapenzi kwa mifugo na ufugaji (tender loving care), sambamba na kuweza kuona fursa za masoko.

Baadhi ya wafugaji  hutazamia kujipatia kipato kikubwa kutoka kwenye mifugo, lakini wameshindwa kuwekeza katika mifugo hiyo ili kuweza kuzalisha kipato hicho. Lazima mfugaji makini ajifunze jinsi ya kuitunza mifugo iweze kumzalishia faida kwa kiwango cha juu.

Ingawa ‘masoko’ ndio jambo la msingi, lakini ‘udhiditi wa magonjwa’, ‘ubora wa chakula’ na ‘mabanda bora’; yote hayo yana umuhimu wake katika ufanisi wa ufugaji.

MABANDA  (housing)

Uhifadhi wa mifugo una changamoto zake kwa mfugaji wa kuku haswa katika ujenzi wa mabanda. Hapa tunaongelea ‘ufugaji huria’ kwa ajili ya kutaga mayai na nyama. Kwa dhana hiyo, mabanda ni lazima yaweze kuhifadhi mifugo dhidi ya baridi kali, upepo mkali na joto kali. Pia ulinzi dhidi ya mbwa, paka pori, panya, nyoka au vicheche ni lazima uzingatiwe. Mabanda yajengwe kwa kutazama upande wa Mashariki, ili kuisaidia mifugo kupata kivuli cha kutosha wakati jua linaelekea upande wa Magharibi. Jua kali au joto kali si zuri sana kwa mifugo hivyo mfugaji anawajibika kuwatengenezea mazingira rafiki yenye kivuli wastani.

Eneo la mita ya mraba MOJA linatosha kwa idadi ya kuku wanaotaga watatu (3) hivyo mfugaji ahakikishe kuna eneo la kutosha ili kupunguza msongamano, unaoweza kusababisha ubabe, kudonoana, ‘stress’ na hata magonjwa. Pia mifugo wanahitaji eneo la wazi nje ya banda kwa ajili ya mapumziko na kustarehe (chicken run area) ili kujipatia hewa safi, kula vijidudu na majani. Eneo la nje ni muhimu sana kwa majogoo kuonyesha umahiri wao. 




Hakikisha viota vya kutagia mayai vinawekwa eneo lisilo na mwanga/ eneo lenye kiziga ili kuku wanaotaga wasionekane kwa uwazi (respect their privacy) na pia kuwa mbali na kuku wengine wataoweza kuwabughudhi wakati wa utagaji. Mfugaji aweke ‘maranda ya mbao’ ndani ya banda na eneo la kutagia, na kuhakikisha hali ya ukavu inadumu ndani ya banda . Zingatia usafi ufanyike kila baada ya siku 4 au 5 ili kuzuia banda kuwa na unyevu, ambao unaweza kupelekea mlipuko wa magonjwa na maambukizi. Upuliziaji wa dawa za kuua wadudu mara kwa mara (spraying of disinfectants) utaongeza tija katika usafi ili kudhibiti vijidudu viambukizavyo magonjwa ndani ya banda. Pia uzingatie yafuatayo;

1. Tumia eneo la ardhi lenye mwanga na kivuli cha wastani kwa ajili ya kujenga banda la mifugo. Eneo live kavu, lenye mawe mawe, ila lisiwe eneo linaloweka maji yanayotuama, tope au eneo linalopitisha maji/ mkondo wa maji wakati wa mvua. Zingatia kuwatenga kuku wanaotaga mayai na wale wanaofugwa kwa kusudi la nyama.

2. Hakikisha upatikanaji wa uhakika wa maji, umeme, chakula na huduma za afya ya mifugo ili kuwa na mazingira rafiki yenye kukidhi mahitaji ya ziada ya mifugo na afya zao.

3. Zingajia kujifunza hadi kupata uzoefu wa kutosha katika ufugaji, kwani kwa kufanya hivyo utaweza kuwa msimamizi mkuu uliyejiridhisha katika shughuli nzima ya ufugaji. Kinyume chake itakuwa rahisi kwa wasaidizi wasio waaminifu kukupa taarifa zisizo sahihi kuhusiana na afya, maendeleo na utagaji wa mifugo yako. Hivyo inakulazimu kutenga muda wa usimamizi makini kwa matendo na sio kwa kupokea taarifa tu.

4. Hakikisha paa la banda lipo imara, kwani uvujifu wa paa utapelekea maji kupenyeza ndani ya banda; na pia hakikisha sakafu nayo ipo imara ili kuzuia maficho ya wadudu kama utitiri, papasi, chawa na maficho ya panya. Mapungufu yeyote ni hatari kwa utunzaji na afya ya mifugo wako. Ikiwa eneo la nje ya banda halina hifadhi ya kivuli, hakikisha unafanya ubunifu wa kuwepo kivuli.

5. Banda linatakiwa kupitisha hewa ya kutosha wakati wote. Urefu wa tofali 3 kutoka kwenye sakafu unafaa zaidi, na paa lichomoze kama futi 3 au 4 zaidi ya usawa wa ukuta ili maji ya mvua yasipate nafasi kupenyeza ndani ya banda kupitia dirishani.

6. Upatikanaji wa mwanga (lighting) ni jambo la kuzingatiwa pia haswa kwa vifaranga, na kuku wanaokua na kuku wanaotaga. Kwani mwezi Julai [ 15 July 2016 ] kuchomoza kwa jua ni saa 12:36 asubuhi; wakati mwezi November [15 Nov 2016] kuchomoza kwa jua ni saa 11:55 asubuhi. Mwezi Januari [ 15 Jan 2016 ] kuzama kwa jua ni saa 12:47 jioni; wakati mwezi Mei [ 15 May 2016 ] kuzama kwa jua ni saa 12:13 jioni.


Hii inamaanisha kuwa kuku wapewe chakula mapema kabla jua halijakuwa kali kwani jua kali/ joto kali litawaathiri. Wakati mwingine nuru ya asubuhi huchelewa kuangaza, haswa miezi ya Februari hadi Julai na Agosti. Hivyo ni muhimu kuratibisha upatikanaji wa mwanga kwaa kusudi la kuipatia mifugo muda wa kutosha wa chakula.

7. Usafi wa banda ni jambo la kuzingatiwa sana, sana, sana ( soma zaidi kwenye Part 3 ya muendelezo wa somo letu ) Hakikisha ‘samadi’/kinyesi chote kinazolewa na kuwekwa mbali na mifugo, kwani inzi wachafu ni wasambazaji wa magonjwa ya mfumo wa tumbo. Ukiweza kuwa na ‘spraying pump’ pamoja na ‘disinfecants’ na kupulizia kwenye mabanda , itaongeza tija sana kuliko usafi wa kawaida tu. Epuka usafi wa kutimua vumbi kwani utalipua ugonjwa wa mafua.

8. Ikiwa unafuga kwa kutumia ‘cages’ ambao ni mfumo wa kudhibiti kinyesi kuwa mbali na kuku, unashauriwa kuwa na utaratibu wa mara kwa mara kunyunyizia majivu au chokaa, na pia kuuondoa uchafu huo, kwa maana uvundo wake utaathiri mzunguko wa hewa na afya ya mifugo kwa ujumla.

9. Ndani mwa banda kubwa, unaweza kuwa mbunifu kujenga vyumba (partition) kwa ajili ya kuwatenga kuku wagonjwa, au majogoo ya hifadhi ‘reserve’, au kuwaweka lock-up matetea usiotaka waatamie kwa wakati huo.

10. Ikiwa unafuga mifugo mingineyo mfano khanga au bata mzinga, tunashauri uiweke katika uhuru wao binafsi ili kujenga utulivu katika utagaji. Kamwe usichanganye au kufuga bata maji karibu na mifugo mingine, kwani maambukizi ya ugonjwa wa typhoid yatakuwa makubwa yakiambatana na hasara kubwa au hata kufa kwa mradi wa ufugaji kuku.

HAYA ndio tumeweza kujifunza leo kwa uchache. Usikose kusoma PART 2 ya muendelezo wa elimu hii ya ufugaji kuku inayoletwa kwako na kwetu.


Sayuni Poultry Gosheni | 0712 057 714 na 0754 282869 | poultrysayuni@gmail.com| Mbezi Mwisho

No comments:

Post a Comment