[Part 2 CHAKULA BORA] MAMBO 4 MUHIMU YA KUKUFANIKISHA KATIKA UFUGAJI KUKU.


Mambo 4 muhimu ya kukufanikisha katika ufugaji kuku. [Part 2]

Kuweza kufanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mfugaji  anahitaji muongozo mzuri na umakini katika MABANDA, CHAKULA BORA, UDHIBITI WA MAGONJWA na MASOKO.

Sehemu ya kwanza [Part 1] imehusu MABANDA  (housing), na sasa tujifunze kuhusu ‘chakula bora’. Ulishaji mifugo ni eneo muhimu zaidi, tena linalohitaji uwekezaji kwani lishe duni itapelekea kipato duni kama sio hasara kabisa.

CHAKULA BORA  (nutritious feeds)

Jinsi ile ile ambavyo mama anamhudumia mwanawe kwa chakula bora katika viwango vya afya yenye ubora (starch, protein, vitamins & fat) ndivyo ambavyo yatupasa kuhudumia mifugo yetu kuanzia vifaranga hadi kuku wanaotaga kwa lengo hilo hilo la KUFIKIA UBORA wa mayai, nyama na uzao wake. Hii inaitwa “Tender loving care. Hatutazamii kupata matokeo chanya kutoka kwenye huduma hasi. Hivyo ni wakati wa KUTHUBUTU. Sisi [Sayuni Poultry Gosheni] tunaamini kuwa ukipata UFAHAMU utakupa KUTHUBUTU, kwani “Unaweza, na tena Inawezekana”.

Katika ufugaji, inaleta tija zaidi pale mfugaji binafsi anapokuwa na uelewa kuhusu chakua cha mifugo. Mfugaji asiye na uelewa huo, inamuwia vigumu kufanya maamuzi inapotokea anahitaji kununua ‘dagaa’ na asiipate huku asijue nini achukue mmbadala ya ‘dagaakwa maana hajui ni nini haswa kinahitajika kwa kuku kutoka kwa hao dagaa. Na hii iwe changamoto binafsi kwa mfugaji kujifunza, kwani hata ikiwa mfugaji amenunua chakua cha mifuko (ready made) na kukatokea mafungufu ya ubora katika utengenezaji chakula hicho, bado mfugaji anatakiwa binafsi awe na uelewa wa chakula bora ili kuisaidia mifugo yake.

Chakula bora kina maeneo makuu ma-nne 1 Wanga /starch; kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu za kiutendaji (ernegy giving food). 2  Protini ; kuimarisha na kuboresha viungo mwilini (build & repair body tissue) 3  Vitamini ; kuimarisha mwili kujikinga dhidi ya magonjwa (increase immunity and protect the body from disease) 4 Mafuta /fat; kuupatia mwili mafuta na nguvu ya kujihifadhi (give the body heat and energy) pamoja na maji safi.

MUHIMU: Inasomeka kuwa vifaranga/kuku wenye umri wa wiki 0 – 6, hupitia kipindi cha kujenga na kuimarisha viungo vyao katika mfumo wa usagaji chakula (Digestive system development) na kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili (Immune system development) hivyo basi, mapungufu yeyote katika ulishaji kwa kipindi hicho, yatapelekea madhara hasi ya kudumu katika maisha ya kuku huyo kwenye mifumo hiyo. Na udhaifu huo wa kuku hautaweza kuimarika kwa kupewa chanjo [ Tafakari:shughulika na msingi kwanza kabla ya kusimamisha jengo la ghorofa, maana ghorofa ikishasimama huwezi tena kuimarisha msingi ulio mbovu” ]

Kipindi cha wiki 6 – 12, kuku hupitia zoezi la kukua, tena kwa haraka ili kupata mwili/umbo kamili la ukuku wake, yaani misuli, mifupa na manyoya. Wengi tunafahamu kuwa ni kipindi mifugo inalishwa chakua cha “Grower” ikimaanisha ukuzaji au ukuaji au kukua. Hiki ni kipindi ambacho kuku, sio kwamba anahitaji chakula bora, bali pia anahitaji chakula kitakachompa ‘stamina’ ya ustahimilivu huko mbeleni. Ustahimilivu wa mifupa na misuli (bones & muscles reserve) utakaomsaidia katika kipindi chake cha juu cha utagaji mayai na ubora wa mayai. Hivyo basi mapungufu yatakayotokea katika ulishaji mifugo kwa kipindi hiki, yatapelekea madhara hasi katika ukuaji wa mifugo yako. Inasomeka kuwa kuku akifikia umri wa wiki 13  anakuwa amekamilisha uimara wa umbo la mifupa (skeleton) kwa 95%, hivyo basi nyongeza yeyote ya chakula au ukuaji haitakuwa na athari (nyongeza au ziada) katika umbo la mifupa. Kipindi hiki cha ukuaji (growth period) inashauriwa sana mfugaji kuwa mwangaifu jinsi anavyoihudumia mifugo yake, ili kupunguza sababisho na uwezekano wa kuchelewesha ukuaji wao. Umakini na utulivu uwepo wakati wa ‘kuwapa chanjo’, ‘kuwahamisha kutoka eneo hadi eneo’, ‘kuwakata midomo’nk, lengo kubwa ni kuwalinda kuku dhidi ya ‘stress’ / masumbufu yeyote yasiyo lazima.

Kipindi cha wiki 12 – 18, kuku huingia kwenye matayarisho ya utagaji. Ni kipindi ambacho misuli inaendelea kukua, hivyo mfugaji uwe mwangalifu katika ulishaji. Maana kwa Majogoo, haswa yaliyokusudiwa kuuzwa kama nyama ni kipindi kizuri kwao kuimarishwa katika lishe itakayowaongezea uzito, misuli na mafuta, lakini kwa matetea waliokusudiwa kutaga mayai, angalizo liwekwe kuzuia ongezeko la uzito na mafuta (excessive body weight & fat pad) Pia izingatiwe kuwa utagaji mayai unaweza kuathiriwa na uzito pungufu kwa kuku na masumbufu (stressfulness) katika utunzaji.

Zingatia yafuatayo;
                                  
1] Tumia chakula chenye viwango vya ubora kwa ajili ya mifugo yako. Usiwe mwepesi kuchukuliwa na maneno ya ushawishi na matangazo ya chakula fulani, badala yake fuatilia na ujiridhishe na majibu chanya kuhusu ubora wa chakula fulani kutoka kwa wafugaji wengine. Inasomeka kuwa vifaranga wa umri wa wiki 0 – 8 wapewe chakula cha ‘Chicks Starter’ au ‘Broiler Starter’ lakini uzoefu unaonyesha kuwa, vifaranga wakifikia umri wa wiki 6 hupendelea chakula chenye punjepunje kubwa zaidi kuliko chakula cha mwanzoni. Hapa unashauriwa kuanza kuchanganya ‘Chicks Starter’ na ‘Broiler Finisher’ . Hii inafanyika ili kuzuia uwezekano wa vifaranga kupunguza ulaji chakula kwa kiwango kinachokusudiwa wao kukua.

Chakula cha Grower mash wapatiwe kuku wakifikia umri wa  wiki 9 – 16, na chakula cha Layer mash wapatiwe wakikifikia wiki ya 17 na kuendelea.

2]   Mfugaji azingatie gharama zote za ulishaji chakula, kwa kuainisha idadi ya mifugo yake sambamba na uwepesi wa kununua chakula au kutengeneza chakula mwenyewe. Mtazamo katika gharama hutofautiana kati ya mfugaji mjasiriamali na mfugaji mwekezaji. Kuku mmoja anayetaga anahitaji chakula bora kwa kiwango cha gramu 130 kwa siku au kilogramu 13 kwa kuku 100 wanaotaga.

3] Chakula cha kuku kiwe kikavu na kihifadhiwe sehemu kavu yenye hewa ya kutosha. Epuka chakula chenye unyevu kwani kitapelekea maambukizi ya fungus. Unashauriwa kuweka ‘coccidiostat’ kwenye chakula chako ili kulinda mifugo dhidi ya ugonjwa wa ‘coccidiosis’ ambao ni hatari kwa mifugo kwa umri wote.

4] Tumia vyombo bora vya chakula vinavyoweza kuhifadhi chakula dhidi ya upotevu wowote au kumwagika. Pia upotevu wa chakula kwa kudhibiti panya waharibifu na wasambazaji magonjwa.

5] Mfugaji azingatie kiwango cha chakula katika ulishaji (adequate feedings ) sawasawa na idadi ya kuku wake ili kudhibiti ongezeko au upungufu wa ulishaji (over or under-feeding) pamoja na kudhibiti uzito wa mifugo.

6] Ulishaji chakula unaweza kuongezeka zaidi ya kiwango kilichotazamiwa kutokana na upotevu wa chakula kupitia vyombo , panya au uduni katika ubora wa chakula. Kiwango cha ulishaji pia kinaweza kupungua kutokana na joto kali, ugonjwa kwa mifugo au chakula kisicho na mvuto (unpalatability).

7] Hakikisha kuku wanapewa chakula fresh, na tena epuka mifugo kukosa chakula kwa muda wa masaa 6 kwani itapelekea kushuka kiwango cha utagaji mayai. Na ikitokea wamekosa chakula kwa masaa 12 itapelekea  athari kubwa katika mfumo wote wa utagaji.

8] Mifugo ipatiwe maji safi na salama kwa muda wote. Usafi uzingatiwe kwenye vyombo vya maji. Hakikisha unatumia chombo cha maji ambacho kuku hawezi kuingia humo na kuchafua maji.

9] Kipindi cha joto kali, hakikisha maji ya kuku yanakuwepo muda wote na vyombo vya maji viwekwe sehemu yenye kivuli ili kuepusha mwanga wa jua kuongeza hali ya joto kwenye maji.

10] Zingatia chanzo cha maji unayowapatia kuku. Mfugaji analazimika kutumia dawa za kutibu maji (disinfecants) dhidi ya vijidudu viletavyo magonjwa aina ya ‘salmonellas

11] Lazima kuzingatia umakini katika upunguzaji wa midomo (debeaking). Kwani mapungufu katika kupunguza midomo yanaweza kupelekea athari katika ulaji, sambamba na utagaji mayai.

12] Jiepushe kufuga mifugo isiyokuwa na tija, mfano matetea yasiyo na sifa ya kutaga au wingi wa majogoo yasiyohitajika. Mifugo hiyo inashauriwa kuchinjwa au kuuzwa.

13] Kuku akikosa uchangamfu katika kula na kunywa maji, ni kiashiria kuwa kuku huyo ni mgonjwa hivyo atengwe mara moja na taratibu za matibabu zianze kuzingatiwa ili kudhibiti maambukizi zaidi na kupelekea vifo.

14] Mfugaji anayetengeneza chakula kwa ajili ya mifugo yake anatakiwa kusimamia kiwango cha wanga (mahindi/mtama) kama msingi wa vipimo vingine. Wafugaji wengine wanatumia kipimo cha ‘gunia la pumba’ kama kigezo cha kujua atahitajika aweke mahindi au dagaa kiasi gani, hiyo sio sawa. Kipimo cha ‘mahindi’ ndio kiwe kigezo cha kupata vipimo vingine, kwa sababu ‘wanga/starch’ ndio yenye sehemu kubwa ya ujazo wa kila aina ya chakula cha kuku. Ongezeko la pumba halipelekei ongezeko la utagaji mayai, bali ni ujazo tu wa makapi ya mlo (fibres).


Endelea kututembelea  [Sayuni Poultry Gosheni] ili ujifunze makala zaidi kuhusu mchanganuo wa utengenezaji wa chakula cha kuku. Tunaamini kuwa itakuwa rahisi kwako mfugaji kujifunza  mchanganuo wa utengenezaji chakula (feeds formula) pale utakapokuwa umejiridhisha kwanza katika ujuzi wa chakula bora (starch, protein, vitamins & fat contents).

Tunakushauri utumie vema eneo la kiwanja chako na ‘nguvu kazi ya nyumbani kwako’ (house-maids au vijana walio likizo za shule au wasio na kazi rasmi) katika kuzalisha kipato zaidi kupitia UFUGAJI na sio kuzalisha gharama.[ Effective use of area and human labour as an ASSET ]


Sayuni Poultry Gosheni | 0712 057 714 na 0754 282 869 | poultrysayuni@gmail.com| Mbezi Mwisho



No comments:

Post a Comment