Mambo 4 muhimu ya
kukufanikisha katika ufugaji kuku. [Part 3]
Kuweza kufanikiwa
katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mfugaji anahitaji muongozo mzuri na umakini katika
MABANDA, CHAKULA BORA, UDHIBITI WA
MAGONJWA na MASOKO.
Sehemu ya tatu [Part 3] inahusu UDHIBITI WA MAGONJWA. Kuku kama viumbe vyote
husumbuliwa na magonjwa kama sehemu ya changamoto za maisha. Mfugaji anawajibika kuitunza mifugo
katika udhibiti wa magonjwa.
UDHIBITI WA MAGONJWA (disease
control & prevention)
Msemo wa “kinga ni bora kuliko tiba” na wenyewe
ni muhimu sana kwa udhibiti wa magonjwa ya mifugo yako. Kama mfugaji unawajibika kujua na kufuata ratiba ya chanjo, ambayo ndio
jambo la kwanza kwa ulinzi wa mifugo dhidi ya magonjwa.
Magonjwa yanaweza kusababishwa na maambukizi
kupitia hewa, au kurithi ugonjwa kupitia wazazi, au uchafu kwenye banda, au
uchafu kwenye vyombo vya maji na chakula, au chakula kilichovunda au kupitia
maambukizi kwa njia ya panya au kuku wa
jirani wasiotunzwa.
Magonjwa huwafanya kuku kuwa dhaifu, husababisha
ukuaji wao kudorora, sambamba na kudorora kwa ulaji wa chakula na utagaji
mayai.
Mfugaji anawajibika kuchunguza ikiwa kuku wake wana
dalili yeyote ya udhaifu au magonjwa. Wakati wa ulishaji, mfugaji anatakiwa
kudadisi ikiwa kuna kuku yeyote asiyechangamka, aliyezubaa, aliyejitenga na
wenzake, mwenye dalili ya kusinzia, mabawa yaliyoshushwa au kusinyaa,
aliyeshusha mkia na aliyejificha kichwa chake ndani mwa mbawa yake. Kuku huyo
ni mgonjwa hivyo atengwe mara moja mbali na wenzake na taratibu za
matibabu zianze kuzingatiwa ili kudhibiti maambukizi zaidi na kupelekea vifo.
Mfugaji anatakiwa kuwasiliana mara moja na wataalam wa mifugo (veterinary personnel)
walio karibu na eneo lake.
[ Tunatambua na kuheshimu elimu ya
wafugaji kwa wafugaji, lakini pia ni vema ujiridhishe kwa kupata jawabu sahihi
kwenye tatizo husika. Kuna kisa cha mfugaji mmoja kushauriwa na mfugaji mwenzake
kuwapatia kuku wanaotaga ‘glucose’ kwa sababu kuku hawezi tu kutembea. Ushauri
huo ulimpelekea hasara badala ya kutatua tatizo husika. Elimu bora ni ile
inayokujuisha ni nini sababisho la tatizo na njia sahihi ya kupata jibu la
tatizo husika. Kwa lugha za mjini wanasema; ‘usitembelee akili ya mwenzako,
bali jiongeze kwa kuchanganya na akili za kwako’
]
Imefahamika kuwa
kuku wanaofugwa kwenye sakafu
wanakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata au kuambukizwa magonjwa. [Sayuni
Poultry Gosheni] Tunakushauri
kuzingatia yafuatayo;
1] Hakikisha unapokea
vifaranga vilivyochangamka kutoka kwa muuzaji, vikiwa vyenye muonekano wa afya
pasipo kuwa na ulemavu wowote wa miguu, mdomo, macho, shingo nk.
2] Fanya ukaguzi mwepesi (sampling test) sehemu ya nyuma ya kifaranga kuhakikisha hakuna ubichi kwenye kitovu. [
makala kamili ya utunzaji wa vifaranga utaisoma kwenye toleo maalum ]
3] Zingatia ratiba ya chanjo
na marudio ya chanjo kwa mifugo yako kuanzia umri wa vifaranga hadi kuku
wakubwa.
4] Hakikicha chanjo ipo
katika ubora wake haswa zile zinazoathirika na hali ya joto. Fuata maelekezo
sahihi ya jinsi ya kuwapa kuku chanjo, kwani zipo chanjo za kuwapa kuku kwa
njia ya maji, au kunyunyizia matone kwenye macho, au za kuchoma kwenye sehemu
ya bawa. Maelekezo ya ziada yazingatiwe kipindi cha joto kali kwani chanjo
inaweza kuharibika mapema.
5] Vifaranga hupewa chanjo ya
‘Newcastle’
katika umri wa siku 7, na hupewa
chanjo ya ‘Gumboro’ katika umri wa siku
14. Marudio ya chanjo ya ‘Newcastle’ hufanyika katika umri wa
siku 21; na marudio ya chanjo ya ‘Gumboro’
hufanyika katika umri wa siku 28.
Kuna chanjo ya ‘Ndui’ ambayo vifaranga
hupewa katika umri wa siku 60 (miezi miwili) . Wasiliana na wataalamu
wa mifugo karibu nawe kuhusu maelekezo ya chanjo.
6] Wiki mbili za kwanza ndizo
zenye changamoto zaidi kwa vifaranga. Mapungufu katika usafi wa vyombo au maji
& chakula kisicho salama ni moja ya sababisho kubwa la magonjwa ya mfumo wa
tumbo kwa vifaranga. Na hii hupelekea mlipuko wa magonjwa yaani miharo na
umajimaji kwenye banda. Mapungufu katika usafi ndani ya banda, haswa kukosekana
kwa mtiririko wa hewa safi, vumbi lililokithiri au unyevunyevu kwenye banda ni
moja ya sababisho kubwa la magonjwa ya mfumo wa hewa kwa vifaranga. Hivyo basi mfugaji anatakiwa kusimamia hali ya
usafi kuanzia chakula, maji, vyombo, banda na hali ya ndani ya banda.
7] Pale imetokea vifaranga
kushambuliwa na magonjwa, ni lazima waendelee na matibabu hadi kumaliza ndipo
wapewe chanjo. Haishauriwi kabisa kukatiza matibabu kwa kusudi la kufuatisha
ratiba ya chanjo. Kumbuka kuwa Elimu haina mwisho, hivyo mfugaji anatakiwa kuzidi kujifunza.
8] Mfugaji unahitajika
kufuatilia hali ya mabadiliko ya hali ya hewa ya eneo husika. Mfano kipindi cha
kiangazi chenye upepo mkali, unashauriwa kuwachanja ‘Newcastle’ ili kuwakinga
mifugo dhidi ya maambukizi kwa njia ya hewa. Na kipindi cha jua/joto kali
unashauriwa kuwapatia maji yenye vitamin (anti-stress) itakayowasaidia
kukabiliana na hali hiyo. Na kipindi cha mvua nyingi, unashauriwa kuitunza
mifugo ndani ya banda katika hali ya usafi wa siku kwa siku, na kinyesi cha
mifugo baada ya kufanya usafi kisiachwe kamwe ndani ya banda.
9] Kutokana na mapungufu
katika usafi kuwa ndio njia kuu mmojawapo ya kupelekea magonjwa kwenye mifugo,
tunashauri kuwa usafi ufanyike mara kwa mara, na mfugaji ajenge tabia ya kunyunyizia dawa za kuua vijidudu (disinfecting/ fumigating) angalau wiki
kwa wiki kwa kusudi la kuua vimelea vya magonjwa, sambamba na kupunguza vumbi
ambalo huweza kuhifadhi bakteria hatarishi kwa mifugo.
10] Zingatia kuwapa mifugo
yako dawa ya minyoo, na marudio yake ni kila baada ya miezi mitatu.
11] Pia unashauriwa kunyunyiza
dawa ya kuua viroboro, chawa, papasi nk kwenye banda la mifugo yako na ikibidi
kuwanyunyizia wao wenyewe. (dusting or spraying) Kusudi ni kuhakikisha
mifugo inadumu katika afya njema na viwango bora vya utagaji.
12] Kwa nia njema tu, epukana
kabisa na watu wageni kwenye eneo lako la ufugaji. Magonjwa ya mifugo huweza
kusambazwa kutoka eneo hadi eneo kupitia wageni waliotoka sehemu nyingine yenye
ufugaji. Pia epuka ugeni wa panya, nao hubeba magonjwa. Unashauriwa kuweka uzio utakaowatenga kuku wako na kuku wa nje wasiotunzwa
13] Mfugo utakayokufa uondolewe
mara moja kutoka kwenye banda na
kuchomwa moto au kuzikwa mbali. Mfugaji
unashauriwa kumtazama mfugo aliyekufa ikiwa sehemu ya kinyesi imechafuka
majimaji au ikiwa ndani ya kinywa ana utando wa kamasi au makohozi. Ufahamu huo
utakusaidia kutoa taarifa sahihi kwa wataalamu au kituo cha matibabu ya mifugo
karibu nawe ili kupata suluhisho sahihi kwa mifugo iliyobaki.
14] Mfugo unaoonyesha dalili
za ugonjwa apatiwe matibabu sahihi na asichinjwe kwa ajili ya chakula au
kuuzwa, kwani lazima kuzingatia afya ya mifugo na zaidi sana afya ya mwanadamu.
15] Ni muhimu sana kudhibiti
magonjwa ya mfumo wa chakula na mfumo wa upumuaji ili kuweza kudumisha
kiwango cha utagaji mayai. Na njia mojawapo ya kudhibiti magonjwa ni kuimarisha
kinga ya mwili ya mifugo yako kwa kuwapatia chakula bora, na ziada ya
chakula (mfano majanimajani, aloe vera
nk)
16] Kinyesi cha mifugo bandani
kinaweza kubeba magonjwa kutoka kuku wa awali kwenda kwa kuku wengine wapya
waingizwao bandani humo. Ni muhimu usafi wa banda na mazingira ufanyike kwa
ufanisi kuweza kuruhusu kuwasili kwa mifugo mingine.
17] Upungufu wa virutubisho
kwenye chakula pia unapelekea magonjwa / madhaifu kwenye mifugo. Kuku kushindwa
kutembea au kuku kuvimba macho huweza kusababishwa na uishaji duni.
18] Usafi ni kiashiria cha
afya njema, na uchafu ni kiashiria cha magonjwa. Hivyo basi usafi ni lazima
uzingatiwe kuanzia kwenye chakula, vyombo vya chakula & maji, mabanda na
mazingira kuzunguka mifugo na usafi kwa mfugaji mwenyewe. KWA MAANA USAFI UNA
UMUHIMU SANA KATIKA HARAKATI NZIMA YA UFUGAJI KUKU.
Endelea
kututembelea [Sayuni
Poultry Gosheni] ili ujifunze makala
zaidi kuhusu aina za magonjwa yanayoshambulia kuku na ushauri wa jinsi ya
kukabiiana nayo.
Tunakushauri utumie vema eneo la kiwanja chako na ‘nguvu kazi ya
nyumbani kwako’ (house-maids au vijana walio likizo za shule au wasio na
kazi rasmi) katika kuzalisha kipato
zaidi kupitia UFUGAJI na sio kuzalisha
gharama.[ Effective use of area and
human labour as an ASSET ]
Sayuni Poultry Gosheni |
0712
057 714 na 0754 282869 |
poultrysayuni@gmail.com|
Mbezi
Mwisho
No comments:
Post a Comment