[Part 4 MASOKO] MAMBO 4 MUHIMU YA KUKUFANIKISHA KATIKA UFUGAJI KUKU.

Mambo 4 muhimu ya kukufanikisha katika ufugaji kuku. [Part 4]

Kuweza kufanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mfugaji  anahitaji muongozo mzuri na umakini katika MABANDA, CHAKULA BORA, UDHIBITI WA MAGONJWA na MASOKO.

MASOKO  (marketing)

Mtazamo kuhusu masoko umekuwa kikwazo kwa wengine kuthubutu kufuga kuku. Hivyo tatizo sio masoko, bali tatizo ni mtazamo. Tujaribu kutathmini wingi wa watu wanaoelekea mjini (Katikati ya Jiji la Dar es Salaam / Dsm City Centre ) wakati wa asubuhi katika siku za kazi  kwa njia ya barabara kupitia makutano ya Tazara, makutano ya Ubungo, makutano ya Morroco, na makutano ya BP/Puma Kurasini, (bila kujumuisha wale wasioelekea Dsm City Centre)
hakika umati huo wote wa watu unahitaji chakula, na kuku ni sehemu ya mlo wa siku.  Wengi sana kati ya umati huo hawafugi kabisa, na hicho ni kiashiria kimojawapo kuwa soko bado lipo na tena ni soko kubwa sana. Ingawa utafutaji wa masoko ‘marketing’ ni taaluma rasmi lakini pia kila mfugaji amejaliwa ubunifu wa jinsi ya kujitafutia masoko. Je kwa nini usifuge ?

Tutafakari yafuatayo;

1] Ufugaji wa nje (nusu huria) ni gharama nafuu kulinganisha na ufugaji wa ndani. Mfugaji atakayeweza kupunguza gharama za ufugaji (kupitia mabanda,chakula bora na udhibiti wa magonjwa) atakuwa na uhuru wa ushindani wa bei sokoni. Tunakushauri utumie vizuri eneo lako la kiwanja kwa kuzalisha faida.



2] Ubora wa mifugo yako, pamoja na uzito sahihi, na afya njema, na mayai yenye sifa yatakupa sauti sokoni kulinganisha na wafugaji wengine.

3] Tunashauri mfugaji afuge kwa malengo. Ikiwa unakusudia kufuga kwa ajili ya nyama basi ni vema ulenge majira au matukio ambayo uhitaji wa kuku unaweza kuwa mkubwa; mfano siku za sikukuu za kidini (Eid, Xmass, Maulid, Pasaka, Ubarikio nk) na pia unaweza kufuatilia sherehe za mahafali vyuoni au mashuleni, pamoja na sherehe za harusi. Usikae kusubiri wateja wakufuate bali peleka taarifa za ubora wa mifugo yako kwenye vikao vya maharusi au migahawa nk,

4] Wajulishe majirani zako kuwa Majogoo/kuku wa ukweli na mayai ya ukweli yanapatikana kwako, kwani sio wote wenye uwezo wa kununua kuku kwa bei ya masokoni. Wakumbushe kuwa wakipata ugeni wa wakwe (Baba au Mama mkwe) ni heshima zaidi wakaandaliwa Jogoo wa ukweli. Habari za ubora wa majogoo yako na mayai yako utajieleza kwa wengine pia.

5] Nyama choma ya nyumbani (iliyoandaliwa kwa viwango vya kuvutia) inaleta mvuto kujenga umoja na upendo wa kifamilia, marafiki na majirani. Mfugaji anaweza kuandaa karamu ya mara kwa mara itakayoambukiza wengine kuwa na ‘jioni ya nyama choma pamoja nyumbani’ yenye ubora bila gharama za ziada. [Home Barbeque]


6] Ukikusudia kuuza mayai, hakikisha kwanza umeona fursa ya wapi utauza mayai yako. Unaweza kujifunza kutoka kwa wafugaji wengine waliokutangulia.

7] Mfugaji anatakiwa kupangilia muda (timing) wa kuuza kuku wake sokoni. Tunamaanisha kuwa usitunze jogoo kwa miezi 7 halafu ukampeleka sokoni kwa bei ambayo ungeweza kumuuza akiwa na miezi 4 - 5. Jogoo wa miezi 7 auzwe kwa bei ya ‘Jogoo wa mbegu’ sawasawa na uhitaji & upatikanaji (demand na supply) wa eneo husika.

8] Mfugaji anaweza kuwa na mradi wa kufuga kuku pamoja na kumiliki mgahawa (au mradi wa familia)  kwenye maeneo na maofisi, vyuo, shule, hospital n.k na kuwa msambazaji wa kuku kwenye mgahawa wako/wa familia.


9] Katika kupata au kufahamu bei ya kuuza mifugo yako, mfugaji unashauriwa kufanya utafiti binafsi wa bei kuweza kujua kuku wanauzwa kwa bei gani. Taarifa hiyo itakusaidia kujua bei elekezi ya kuuzia sokoni. Unaweza kutembelea masoko sehemu kwa sehemu uweze kupata bei ya kuuzia yenye faida zaidi kwako ( bei ya jogoo kwenye soko eneo la Mwenge ni tofauti na soko eneo la Kimara )

10] Kuweza kupata tenda ya kuuza kuku kwenye mahoteli au migahawa mikubwa, mfugaji anashauriwa kuwa kwenye kikundi cha ushirika (umoja wa wafugaji au saccos au vicoba au  umoja wa wajasiriamali wanafunzi waliopo chuoni au akina mama majirani) kwa kusudi la kuweza ku-supply kiwango cha kuku kinachohitajika pasipo kuwa na mapungufu (reliable supply). Umoja utapelekea uwajibikaji kwa kila mfugaji na hatimae kuleta ufanisi katika mradi wa ufugaji kuku.

Soko la uhakika linapatikana pale mfugaji anapoweza kutumia fursa na kushinda changamoto za mtazamo. Sisi [Sayuni Poultry Gosheni] tunaamini kuwa “Unaweza, na tena Inawezekana”.

___________________________________________________________________________

Tunakushauri utumie vema eneo la kiwanja chako na ‘nguvu kazi ya nyumbani kwako’ (house-maids au vijana walio likizo za shule au wasio na kazi rasmi) katika kuzalisha kipato zaidi kupitia UFUGAJI na sio kuzalisha gharama.[ Effective use of area and human labour as an ASSET ]


Sayuni Poultry Gosheni | 0712 057 714 na 0754 282869 | poultrysayuni@gmail.com| Mbezi Mwisho

___________________________________________________________________________


No comments:

Post a Comment