UTUNZAJI VIFARANGA KWENYE ARDHI, KWA KUTUMIA JOTO NA MWANGA WA JUA

Kutoka ‘SAYUNI POULTRY GOSHENI’ pekee tunakuletea UTUNZAJI wa VIFARANGA ulio mwepesi kabisa tena wa gharama nafuu kabisa.

Hii sio ELIMU, bali ni ubunifu tu utakaokuwezesha kuvuka na kupiga hatua. Utunzaji vifaranga nao umekuwa changamoto kwa wafugaji wachanga ambao wengi wametawaliwa na hofu ya kupata hasara. Hebu tujifunze pamoja.

Pichani hapo chini ni picha ya banda (simple & local designed) lenye urefu wa inchi 50 na upana wa inchi 27 na kimo ni inchi 12. Limefunikwa chick-wire-mash upande wa juu na pembezoni, ila kwa chini liko wazi, chini ni ARDHI, ni mchanga / udongo. UKIPATA FUNDI MWAMINIFU AU UKIJISHUGHULISHA BINAFSI, GHARAMA YAKE HAIZIDI 15,000= au 20,000= ambayo ni faida sana ukilinganisha na gharama ya dawa, na ni faida zaidi ikiwa utatunza vifaranga mara kwa mara.



Katika wiki mbili za mwanzo vifaranga hushambuliwa sana na magonjwa ya mafua na/au miharo ambayo yote husababishwa na uchafu kwenye mabanda. Na pia wiki mbili za mwanzo, vifaranga huhitaji joto la kutosha kwa masaa yote 24 ya siku.

Ninapotumia utunzaji huu; kwanza kabisa vifaranga vinapata HEWA halisi (free fresh air) moja kwa moja, tena vinafurahia MWANGA na JOTO la JUA moja kwa moja, halafu vinafurahia ile ARDHI, kwani kwao ni mpya/fresh kila siku (haina muendelezo wa kinyesi cha juzi wala jana) na tena vifaranga hupendelea KUOGA kwenye mchanga (sand-bathing). Vifaranga huwa salama dhidi ya kunguru nap aka na muda wote huonekana machoni pako/mtunzaji (visible observed).

Wakati JUA limekuwa kali sana, watengenezee KIVULI, (nusu KIVULI, nusu JUA, ili kuweza kupata joto la wastani na mwanga wa wastani) ila hakikisha HEWA ya kutosha inaingia. Usiogope ‘hasara’ ni sehemu ya kujifunza kutokana na makossa, ambayo next time/mara nyingine utakuwa umeelimika.

Kwa utunzaji huu ‘simple & natural’, hakuna namna itakayopelekea kutumia dawa za mafua au miharo na pia gharama za nishati (joto na mwanga) zitashuka. Wakati wa usiku, italazimu kuvirudisha vifaranga vyako kwenye banda la ndani au kwenye box. Zingatia USAFI, DAWA za KUANZIA na ratiba ya CHANJO muhimu.

Jipatie “VIFARANGA 30” kwa bei ya OFA, na uweze KUTUNZA VIFARANGA vyako kwa UHAKIKA kabisa.
Kumbuka “VIFARANGA 30” ni UHAKIKA kulinganisha na KUTOTOLESHA MAYAI 30 kwani haukupi UHAKIKA wa idadi ya vifaranga.

Ukipata “VIFARANGA 30” kwa UHAKIKA na elimu ya UTUNZAJI vifaranga kwa UHAKIKA hukupa MATOKEO ya UHAKIKA katika UFUGAJI. 


Ni wapi hapo? ni ‘SAYUNI POULTRY GOSHENI’ pekee inayokupatia # VIFARANGA na tena # ELIMU ya UTUNZAJI VIFARANGA bure, na tena # UTOTOLESHAJI wa MAYAI yako, na tena # ELIMU ya UTOTOLESHAJI bure, na tena # OFA za UTOTOLESHAJI, na tena # USHAURI wa MIFUGO bure, na tena # HUDUMA kwa WATEJA bure kwa njia ya simu, na tena # Mambo mengine meeeengi… .


…usisite kumjulisha na jirani/rafiki/jamaa zako. Soma makala kamili ya UTUNZAJI VIFARANGA.

[Part 4 MASOKO] MAMBO 4 MUHIMU YA KUKUFANIKISHA KATIKA UFUGAJI KUKU.

Mambo 4 muhimu ya kukufanikisha katika ufugaji kuku. [Part 4]

Kuweza kufanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mfugaji  anahitaji muongozo mzuri na umakini katika MABANDA, CHAKULA BORA, UDHIBITI WA MAGONJWA na MASOKO.

MASOKO  (marketing)

Mtazamo kuhusu masoko umekuwa kikwazo kwa wengine kuthubutu kufuga kuku. Hivyo tatizo sio masoko, bali tatizo ni mtazamo. Tujaribu kutathmini wingi wa watu wanaoelekea mjini (Katikati ya Jiji la Dar es Salaam / Dsm City Centre ) wakati wa asubuhi katika siku za kazi  kwa njia ya barabara kupitia makutano ya Tazara, makutano ya Ubungo, makutano ya Morroco, na makutano ya BP/Puma Kurasini, (bila kujumuisha wale wasioelekea Dsm City Centre)
hakika umati huo wote wa watu unahitaji chakula, na kuku ni sehemu ya mlo wa siku.  Wengi sana kati ya umati huo hawafugi kabisa, na hicho ni kiashiria kimojawapo kuwa soko bado lipo na tena ni soko kubwa sana. Ingawa utafutaji wa masoko ‘marketing’ ni taaluma rasmi lakini pia kila mfugaji amejaliwa ubunifu wa jinsi ya kujitafutia masoko. Je kwa nini usifuge ?

Tutafakari yafuatayo;

1] Ufugaji wa nje (nusu huria) ni gharama nafuu kulinganisha na ufugaji wa ndani. Mfugaji atakayeweza kupunguza gharama za ufugaji (kupitia mabanda,chakula bora na udhibiti wa magonjwa) atakuwa na uhuru wa ushindani wa bei sokoni. Tunakushauri utumie vizuri eneo lako la kiwanja kwa kuzalisha faida.



2] Ubora wa mifugo yako, pamoja na uzito sahihi, na afya njema, na mayai yenye sifa yatakupa sauti sokoni kulinganisha na wafugaji wengine.

3] Tunashauri mfugaji afuge kwa malengo. Ikiwa unakusudia kufuga kwa ajili ya nyama basi ni vema ulenge majira au matukio ambayo uhitaji wa kuku unaweza kuwa mkubwa; mfano siku za sikukuu za kidini (Eid, Xmass, Maulid, Pasaka, Ubarikio nk) na pia unaweza kufuatilia sherehe za mahafali vyuoni au mashuleni, pamoja na sherehe za harusi. Usikae kusubiri wateja wakufuate bali peleka taarifa za ubora wa mifugo yako kwenye vikao vya maharusi au migahawa nk,

4] Wajulishe majirani zako kuwa Majogoo/kuku wa ukweli na mayai ya ukweli yanapatikana kwako, kwani sio wote wenye uwezo wa kununua kuku kwa bei ya masokoni. Wakumbushe kuwa wakipata ugeni wa wakwe (Baba au Mama mkwe) ni heshima zaidi wakaandaliwa Jogoo wa ukweli. Habari za ubora wa majogoo yako na mayai yako utajieleza kwa wengine pia.

5] Nyama choma ya nyumbani (iliyoandaliwa kwa viwango vya kuvutia) inaleta mvuto kujenga umoja na upendo wa kifamilia, marafiki na majirani. Mfugaji anaweza kuandaa karamu ya mara kwa mara itakayoambukiza wengine kuwa na ‘jioni ya nyama choma pamoja nyumbani’ yenye ubora bila gharama za ziada. [Home Barbeque]


6] Ukikusudia kuuza mayai, hakikisha kwanza umeona fursa ya wapi utauza mayai yako. Unaweza kujifunza kutoka kwa wafugaji wengine waliokutangulia.

7] Mfugaji anatakiwa kupangilia muda (timing) wa kuuza kuku wake sokoni. Tunamaanisha kuwa usitunze jogoo kwa miezi 7 halafu ukampeleka sokoni kwa bei ambayo ungeweza kumuuza akiwa na miezi 4 - 5. Jogoo wa miezi 7 auzwe kwa bei ya ‘Jogoo wa mbegu’ sawasawa na uhitaji & upatikanaji (demand na supply) wa eneo husika.

8] Mfugaji anaweza kuwa na mradi wa kufuga kuku pamoja na kumiliki mgahawa (au mradi wa familia)  kwenye maeneo na maofisi, vyuo, shule, hospital n.k na kuwa msambazaji wa kuku kwenye mgahawa wako/wa familia.


9] Katika kupata au kufahamu bei ya kuuza mifugo yako, mfugaji unashauriwa kufanya utafiti binafsi wa bei kuweza kujua kuku wanauzwa kwa bei gani. Taarifa hiyo itakusaidia kujua bei elekezi ya kuuzia sokoni. Unaweza kutembelea masoko sehemu kwa sehemu uweze kupata bei ya kuuzia yenye faida zaidi kwako ( bei ya jogoo kwenye soko eneo la Mwenge ni tofauti na soko eneo la Kimara )

10] Kuweza kupata tenda ya kuuza kuku kwenye mahoteli au migahawa mikubwa, mfugaji anashauriwa kuwa kwenye kikundi cha ushirika (umoja wa wafugaji au saccos au vicoba au  umoja wa wajasiriamali wanafunzi waliopo chuoni au akina mama majirani) kwa kusudi la kuweza ku-supply kiwango cha kuku kinachohitajika pasipo kuwa na mapungufu (reliable supply). Umoja utapelekea uwajibikaji kwa kila mfugaji na hatimae kuleta ufanisi katika mradi wa ufugaji kuku.

Soko la uhakika linapatikana pale mfugaji anapoweza kutumia fursa na kushinda changamoto za mtazamo. Sisi [Sayuni Poultry Gosheni] tunaamini kuwa “Unaweza, na tena Inawezekana”.

___________________________________________________________________________

Tunakushauri utumie vema eneo la kiwanja chako na ‘nguvu kazi ya nyumbani kwako’ (house-maids au vijana walio likizo za shule au wasio na kazi rasmi) katika kuzalisha kipato zaidi kupitia UFUGAJI na sio kuzalisha gharama.[ Effective use of area and human labour as an ASSET ]


Sayuni Poultry Gosheni | 0712 057 714 na 0754 282869 | poultrysayuni@gmail.com| Mbezi Mwisho

___________________________________________________________________________


[Part 3 UDHIBITI WA MAGONJWA] MAMBO 4 MUHIMU YA KUKUFANIKISHA KATIKA UFUGAJI KUKU.

Mambo 4 muhimu ya kukufanikisha katika ufugaji kuku. [Part 3]

Kuweza kufanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mfugaji  anahitaji muongozo mzuri na umakini katika MABANDA, CHAKULA BORA, UDHIBITI WA MAGONJWA na MASOKO.

Sehemu ya tatu [Part 3] inahusu UDHIBITI WA MAGONJWA. Kuku kama viumbe vyote husumbuliwa na magonjwa kama sehemu ya changamoto za maisha. Mfugaji anawajibika kuitunza mifugo katika udhibiti wa magonjwa.

UDHIBITI WA MAGONJWA  (disease control & prevention)

Msemo wa “kinga ni bora kuliko tiba” na wenyewe ni muhimu sana kwa udhibiti wa magonjwa ya mifugo yako. Kama mfugaji unawajibika kujua  na kufuata ratiba ya chanjo, ambayo ndio jambo la kwanza kwa ulinzi wa mifugo dhidi ya magonjwa.

Magonjwa yanaweza kusababishwa na maambukizi kupitia hewa, au kurithi ugonjwa kupitia wazazi, au uchafu kwenye banda, au uchafu kwenye vyombo vya maji na chakula, au chakula kilichovunda au kupitia maambukizi kwa njia ya panya au kuku wa jirani wasiotunzwa. 



Magonjwa huwafanya kuku kuwa dhaifu, husababisha ukuaji wao kudorora, sambamba na kudorora kwa ulaji wa chakula na utagaji mayai.

Mfugaji anawajibika kuchunguza ikiwa kuku wake wana dalili yeyote ya udhaifu au magonjwa. Wakati wa ulishaji, mfugaji anatakiwa kudadisi ikiwa kuna kuku yeyote asiyechangamka, aliyezubaa, aliyejitenga na wenzake, mwenye dalili ya kusinzia, mabawa yaliyoshushwa au kusinyaa, aliyeshusha mkia na aliyejificha kichwa chake ndani mwa mbawa yake. Kuku huyo ni mgonjwa hivyo atengwe mara moja mbali na wenzake na taratibu za matibabu zianze kuzingatiwa ili kudhibiti maambukizi zaidi na kupelekea vifo. Mfugaji anatakiwa kuwasiliana mara moja na wataalam wa mifugo (veterinary personnel) walio karibu na eneo lake.

[ Tunatambua na kuheshimu elimu ya wafugaji kwa wafugaji, lakini pia ni vema ujiridhishe kwa kupata jawabu sahihi kwenye tatizo husika. Kuna kisa cha mfugaji mmoja kushauriwa na mfugaji mwenzake kuwapatia kuku wanaotaga ‘glucose’ kwa sababu kuku hawezi tu kutembea. Ushauri huo ulimpelekea hasara badala ya kutatua tatizo husika. Elimu bora ni ile inayokujuisha ni nini sababisho la tatizo na njia sahihi ya kupata jibu la tatizo husika. Kwa lugha za mjini wanasema; ‘usitembelee akili ya mwenzako, bali jiongeze kwa kuchanganya na akili za kwako’ ]

Imefahamika kuwa kuku wanaofugwa kwenye sakafu wanakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata au kuambukizwa magonjwa. [Sayuni Poultry Gosheni] Tunakushauri kuzingatia yafuatayo;

1] Hakikisha unapokea vifaranga vilivyochangamka kutoka kwa muuzaji, vikiwa vyenye muonekano wa afya pasipo kuwa na ulemavu wowote wa miguu, mdomo, macho, shingo nk. 


2] Fanya ukaguzi mwepesi (sampling test) sehemu ya nyuma ya kifaranga kuhakikisha hakuna ubichi kwenye kitovu. [ makala kamili ya utunzaji wa vifaranga utaisoma kwenye toleo maalum ]

3] Zingatia ratiba ya chanjo na marudio ya chanjo kwa mifugo yako kuanzia umri wa vifaranga hadi kuku wakubwa.
4] Hakikicha chanjo ipo katika ubora wake haswa zile zinazoathirika na hali ya joto. Fuata maelekezo sahihi ya jinsi ya kuwapa kuku chanjo, kwani zipo chanjo za kuwapa kuku kwa njia ya maji, au kunyunyizia matone kwenye macho, au za kuchoma kwenye sehemu ya bawa. Maelekezo ya ziada yazingatiwe kipindi cha joto kali kwani chanjo inaweza kuharibika mapema.

5] Vifaranga hupewa chanjo ya ‘Newcastle’ katika umri wa siku 7, na hupewa chanjo ya ‘Gumboro’ katika umri wa siku 14. Marudio ya chanjo ya ‘Newcastle’ hufanyika katika umri wa siku 21; na marudio ya chanjo ya ‘Gumboro’ hufanyika katika umri wa siku 28. Kuna chanjo ya ‘Ndui’  ambayo vifaranga hupewa katika umri wa siku 60 (miezi miwili) . Wasiliana na wataalamu wa mifugo karibu nawe kuhusu maelekezo ya chanjo.

6] Wiki mbili za kwanza ndizo zenye changamoto zaidi kwa vifaranga. Mapungufu katika usafi wa vyombo au maji & chakula kisicho salama ni moja ya sababisho kubwa la magonjwa ya mfumo wa tumbo kwa vifaranga. Na hii hupelekea mlipuko wa magonjwa yaani miharo na umajimaji kwenye banda. Mapungufu katika usafi ndani ya banda, haswa kukosekana kwa mtiririko wa hewa safi, vumbi lililokithiri au unyevunyevu kwenye banda ni moja ya sababisho kubwa la magonjwa ya mfumo wa hewa kwa vifaranga. Hivyo basi mfugaji anatakiwa kusimamia hali ya usafi kuanzia chakula, maji, vyombo, banda na hali ya ndani ya banda.

7] Pale imetokea vifaranga kushambuliwa na magonjwa, ni lazima waendelee na matibabu hadi kumaliza ndipo wapewe chanjo. Haishauriwi kabisa kukatiza matibabu kwa kusudi la kufuatisha ratiba ya chanjo. Kumbuka kuwa Elimu haina mwisho, hivyo mfugaji anatakiwa kuzidi kujifunza.

8] Mfugaji unahitajika kufuatilia hali ya mabadiliko ya hali ya hewa ya eneo husika. Mfano kipindi cha kiangazi chenye upepo mkali, unashauriwa kuwachanja ‘Newcastle’ ili kuwakinga mifugo dhidi ya maambukizi kwa njia ya hewa. Na kipindi cha jua/joto kali unashauriwa kuwapatia maji yenye vitamin (anti-stress) itakayowasaidia kukabiliana na hali hiyo. Na kipindi cha mvua nyingi, unashauriwa kuitunza mifugo ndani ya banda katika hali ya usafi wa siku kwa siku, na kinyesi cha mifugo baada ya kufanya usafi kisiachwe kamwe ndani ya banda.

9] Kutokana na mapungufu katika usafi kuwa ndio njia kuu mmojawapo ya kupelekea magonjwa kwenye mifugo, tunashauri kuwa usafi ufanyike mara kwa mara, na mfugaji ajenge tabia ya kunyunyizia dawa za kuua vijidudu (disinfecting/ fumigating) angalau wiki kwa wiki kwa kusudi la kuua vimelea vya magonjwa, sambamba na kupunguza vumbi ambalo huweza kuhifadhi bakteria hatarishi kwa mifugo.

10] Zingatia kuwapa mifugo yako dawa ya minyoo, na marudio yake ni kila baada ya miezi mitatu.

11] Pia unashauriwa kunyunyiza dawa ya kuua viroboro, chawa, papasi nk kwenye banda la mifugo yako na ikibidi kuwanyunyizia wao wenyewe. (dusting or spraying) Kusudi ni kuhakikisha mifugo inadumu katika afya njema na viwango bora vya utagaji.

12] Kwa nia njema tu, epukana kabisa na watu wageni kwenye eneo lako la ufugaji. Magonjwa ya mifugo huweza kusambazwa kutoka eneo hadi eneo kupitia wageni waliotoka sehemu nyingine yenye ufugaji. Pia epuka ugeni wa panya, nao hubeba magonjwa. Unashauriwa kuweka uzio utakaowatenga kuku wako na kuku wa nje wasiotunzwa




13] Mfugo utakayokufa uondolewe mara moja  kutoka kwenye banda na kuchomwa moto au kuzikwa mbali. Mfugaji unashauriwa kumtazama mfugo aliyekufa ikiwa sehemu ya kinyesi imechafuka majimaji au ikiwa ndani ya kinywa ana utando wa kamasi au makohozi. Ufahamu huo utakusaidia kutoa taarifa sahihi kwa wataalamu au kituo cha matibabu ya mifugo karibu nawe ili kupata suluhisho sahihi kwa mifugo iliyobaki.

14] Mfugo unaoonyesha dalili za ugonjwa apatiwe matibabu sahihi na asichinjwe kwa ajili ya chakula au kuuzwa, kwani lazima kuzingatia afya ya mifugo na zaidi sana afya ya mwanadamu.

15] Ni muhimu sana kudhibiti magonjwa ya mfumo wa chakula na mfumo wa upumuaji ili kuweza kudumisha kiwango cha utagaji mayai. Na njia mojawapo ya kudhibiti magonjwa ni kuimarisha kinga ya mwili ya mifugo yako kwa kuwapatia chakula bora, na ziada ya chakula (mfano majanimajani, aloe vera nk)

16] Kinyesi cha mifugo bandani kinaweza kubeba magonjwa kutoka kuku wa awali kwenda kwa kuku wengine wapya waingizwao bandani humo. Ni muhimu usafi wa banda na mazingira ufanyike kwa ufanisi kuweza kuruhusu kuwasili kwa mifugo mingine.

17] Upungufu wa virutubisho kwenye chakula pia unapelekea magonjwa / madhaifu kwenye mifugo. Kuku kushindwa kutembea au kuku kuvimba macho huweza kusababishwa na uishaji duni.

18] Usafi ni kiashiria cha afya njema, na uchafu ni kiashiria cha magonjwa. Hivyo basi usafi ni lazima uzingatiwe kuanzia kwenye chakula, vyombo vya chakula & maji, mabanda na mazingira kuzunguka mifugo na usafi kwa mfugaji mwenyewe. KWA MAANA USAFI UNA UMUHIMU SANA KATIKA HARAKATI NZIMA YA UFUGAJI KUKU.



Endelea kututembelea  [Sayuni Poultry Gosheni] ili ujifunze makala zaidi kuhusu aina za magonjwa yanayoshambulia kuku na ushauri wa jinsi ya kukabiiana nayo.

Tunakushauri utumie vema eneo la kiwanja chako na ‘nguvu kazi ya nyumbani kwako’ (house-maids au vijana walio likizo za shule au wasio na kazi rasmi) katika kuzalisha kipato zaidi kupitia UFUGAJI na sio kuzalisha gharama.[ Effective use of area and human labour as an ASSET ]


Sayuni Poultry Gosheni | 0712 057 714 na 0754 282869 | poultrysayuni@gmail.com| Mbezi Mwisho




[Part 2 CHAKULA BORA] MAMBO 4 MUHIMU YA KUKUFANIKISHA KATIKA UFUGAJI KUKU.


Mambo 4 muhimu ya kukufanikisha katika ufugaji kuku. [Part 2]

Kuweza kufanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mfugaji  anahitaji muongozo mzuri na umakini katika MABANDA, CHAKULA BORA, UDHIBITI WA MAGONJWA na MASOKO.

Sehemu ya kwanza [Part 1] imehusu MABANDA  (housing), na sasa tujifunze kuhusu ‘chakula bora’. Ulishaji mifugo ni eneo muhimu zaidi, tena linalohitaji uwekezaji kwani lishe duni itapelekea kipato duni kama sio hasara kabisa.

CHAKULA BORA  (nutritious feeds)

Jinsi ile ile ambavyo mama anamhudumia mwanawe kwa chakula bora katika viwango vya afya yenye ubora (starch, protein, vitamins & fat) ndivyo ambavyo yatupasa kuhudumia mifugo yetu kuanzia vifaranga hadi kuku wanaotaga kwa lengo hilo hilo la KUFIKIA UBORA wa mayai, nyama na uzao wake. Hii inaitwa “Tender loving care. Hatutazamii kupata matokeo chanya kutoka kwenye huduma hasi. Hivyo ni wakati wa KUTHUBUTU. Sisi [Sayuni Poultry Gosheni] tunaamini kuwa ukipata UFAHAMU utakupa KUTHUBUTU, kwani “Unaweza, na tena Inawezekana”.

Katika ufugaji, inaleta tija zaidi pale mfugaji binafsi anapokuwa na uelewa kuhusu chakua cha mifugo. Mfugaji asiye na uelewa huo, inamuwia vigumu kufanya maamuzi inapotokea anahitaji kununua ‘dagaa’ na asiipate huku asijue nini achukue mmbadala ya ‘dagaakwa maana hajui ni nini haswa kinahitajika kwa kuku kutoka kwa hao dagaa. Na hii iwe changamoto binafsi kwa mfugaji kujifunza, kwani hata ikiwa mfugaji amenunua chakua cha mifuko (ready made) na kukatokea mafungufu ya ubora katika utengenezaji chakula hicho, bado mfugaji anatakiwa binafsi awe na uelewa wa chakula bora ili kuisaidia mifugo yake.

Chakula bora kina maeneo makuu ma-nne 1 Wanga /starch; kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu za kiutendaji (ernegy giving food). 2  Protini ; kuimarisha na kuboresha viungo mwilini (build & repair body tissue) 3  Vitamini ; kuimarisha mwili kujikinga dhidi ya magonjwa (increase immunity and protect the body from disease) 4 Mafuta /fat; kuupatia mwili mafuta na nguvu ya kujihifadhi (give the body heat and energy) pamoja na maji safi.

MUHIMU: Inasomeka kuwa vifaranga/kuku wenye umri wa wiki 0 – 6, hupitia kipindi cha kujenga na kuimarisha viungo vyao katika mfumo wa usagaji chakula (Digestive system development) na kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili (Immune system development) hivyo basi, mapungufu yeyote katika ulishaji kwa kipindi hicho, yatapelekea madhara hasi ya kudumu katika maisha ya kuku huyo kwenye mifumo hiyo. Na udhaifu huo wa kuku hautaweza kuimarika kwa kupewa chanjo [ Tafakari:shughulika na msingi kwanza kabla ya kusimamisha jengo la ghorofa, maana ghorofa ikishasimama huwezi tena kuimarisha msingi ulio mbovu” ]

Kipindi cha wiki 6 – 12, kuku hupitia zoezi la kukua, tena kwa haraka ili kupata mwili/umbo kamili la ukuku wake, yaani misuli, mifupa na manyoya. Wengi tunafahamu kuwa ni kipindi mifugo inalishwa chakua cha “Grower” ikimaanisha ukuzaji au ukuaji au kukua. Hiki ni kipindi ambacho kuku, sio kwamba anahitaji chakula bora, bali pia anahitaji chakula kitakachompa ‘stamina’ ya ustahimilivu huko mbeleni. Ustahimilivu wa mifupa na misuli (bones & muscles reserve) utakaomsaidia katika kipindi chake cha juu cha utagaji mayai na ubora wa mayai. Hivyo basi mapungufu yatakayotokea katika ulishaji mifugo kwa kipindi hiki, yatapelekea madhara hasi katika ukuaji wa mifugo yako. Inasomeka kuwa kuku akifikia umri wa wiki 13  anakuwa amekamilisha uimara wa umbo la mifupa (skeleton) kwa 95%, hivyo basi nyongeza yeyote ya chakula au ukuaji haitakuwa na athari (nyongeza au ziada) katika umbo la mifupa. Kipindi hiki cha ukuaji (growth period) inashauriwa sana mfugaji kuwa mwangaifu jinsi anavyoihudumia mifugo yake, ili kupunguza sababisho na uwezekano wa kuchelewesha ukuaji wao. Umakini na utulivu uwepo wakati wa ‘kuwapa chanjo’, ‘kuwahamisha kutoka eneo hadi eneo’, ‘kuwakata midomo’nk, lengo kubwa ni kuwalinda kuku dhidi ya ‘stress’ / masumbufu yeyote yasiyo lazima.

Kipindi cha wiki 12 – 18, kuku huingia kwenye matayarisho ya utagaji. Ni kipindi ambacho misuli inaendelea kukua, hivyo mfugaji uwe mwangalifu katika ulishaji. Maana kwa Majogoo, haswa yaliyokusudiwa kuuzwa kama nyama ni kipindi kizuri kwao kuimarishwa katika lishe itakayowaongezea uzito, misuli na mafuta, lakini kwa matetea waliokusudiwa kutaga mayai, angalizo liwekwe kuzuia ongezeko la uzito na mafuta (excessive body weight & fat pad) Pia izingatiwe kuwa utagaji mayai unaweza kuathiriwa na uzito pungufu kwa kuku na masumbufu (stressfulness) katika utunzaji.

Zingatia yafuatayo;
                                  
1] Tumia chakula chenye viwango vya ubora kwa ajili ya mifugo yako. Usiwe mwepesi kuchukuliwa na maneno ya ushawishi na matangazo ya chakula fulani, badala yake fuatilia na ujiridhishe na majibu chanya kuhusu ubora wa chakula fulani kutoka kwa wafugaji wengine. Inasomeka kuwa vifaranga wa umri wa wiki 0 – 8 wapewe chakula cha ‘Chicks Starter’ au ‘Broiler Starter’ lakini uzoefu unaonyesha kuwa, vifaranga wakifikia umri wa wiki 6 hupendelea chakula chenye punjepunje kubwa zaidi kuliko chakula cha mwanzoni. Hapa unashauriwa kuanza kuchanganya ‘Chicks Starter’ na ‘Broiler Finisher’ . Hii inafanyika ili kuzuia uwezekano wa vifaranga kupunguza ulaji chakula kwa kiwango kinachokusudiwa wao kukua.

Chakula cha Grower mash wapatiwe kuku wakifikia umri wa  wiki 9 – 16, na chakula cha Layer mash wapatiwe wakikifikia wiki ya 17 na kuendelea.

2]   Mfugaji azingatie gharama zote za ulishaji chakula, kwa kuainisha idadi ya mifugo yake sambamba na uwepesi wa kununua chakula au kutengeneza chakula mwenyewe. Mtazamo katika gharama hutofautiana kati ya mfugaji mjasiriamali na mfugaji mwekezaji. Kuku mmoja anayetaga anahitaji chakula bora kwa kiwango cha gramu 130 kwa siku au kilogramu 13 kwa kuku 100 wanaotaga.

3] Chakula cha kuku kiwe kikavu na kihifadhiwe sehemu kavu yenye hewa ya kutosha. Epuka chakula chenye unyevu kwani kitapelekea maambukizi ya fungus. Unashauriwa kuweka ‘coccidiostat’ kwenye chakula chako ili kulinda mifugo dhidi ya ugonjwa wa ‘coccidiosis’ ambao ni hatari kwa mifugo kwa umri wote.

4] Tumia vyombo bora vya chakula vinavyoweza kuhifadhi chakula dhidi ya upotevu wowote au kumwagika. Pia upotevu wa chakula kwa kudhibiti panya waharibifu na wasambazaji magonjwa.

5] Mfugaji azingatie kiwango cha chakula katika ulishaji (adequate feedings ) sawasawa na idadi ya kuku wake ili kudhibiti ongezeko au upungufu wa ulishaji (over or under-feeding) pamoja na kudhibiti uzito wa mifugo.

6] Ulishaji chakula unaweza kuongezeka zaidi ya kiwango kilichotazamiwa kutokana na upotevu wa chakula kupitia vyombo , panya au uduni katika ubora wa chakula. Kiwango cha ulishaji pia kinaweza kupungua kutokana na joto kali, ugonjwa kwa mifugo au chakula kisicho na mvuto (unpalatability).

7] Hakikisha kuku wanapewa chakula fresh, na tena epuka mifugo kukosa chakula kwa muda wa masaa 6 kwani itapelekea kushuka kiwango cha utagaji mayai. Na ikitokea wamekosa chakula kwa masaa 12 itapelekea  athari kubwa katika mfumo wote wa utagaji.

8] Mifugo ipatiwe maji safi na salama kwa muda wote. Usafi uzingatiwe kwenye vyombo vya maji. Hakikisha unatumia chombo cha maji ambacho kuku hawezi kuingia humo na kuchafua maji.

9] Kipindi cha joto kali, hakikisha maji ya kuku yanakuwepo muda wote na vyombo vya maji viwekwe sehemu yenye kivuli ili kuepusha mwanga wa jua kuongeza hali ya joto kwenye maji.

10] Zingatia chanzo cha maji unayowapatia kuku. Mfugaji analazimika kutumia dawa za kutibu maji (disinfecants) dhidi ya vijidudu viletavyo magonjwa aina ya ‘salmonellas

11] Lazima kuzingatia umakini katika upunguzaji wa midomo (debeaking). Kwani mapungufu katika kupunguza midomo yanaweza kupelekea athari katika ulaji, sambamba na utagaji mayai.

12] Jiepushe kufuga mifugo isiyokuwa na tija, mfano matetea yasiyo na sifa ya kutaga au wingi wa majogoo yasiyohitajika. Mifugo hiyo inashauriwa kuchinjwa au kuuzwa.

13] Kuku akikosa uchangamfu katika kula na kunywa maji, ni kiashiria kuwa kuku huyo ni mgonjwa hivyo atengwe mara moja na taratibu za matibabu zianze kuzingatiwa ili kudhibiti maambukizi zaidi na kupelekea vifo.

14] Mfugaji anayetengeneza chakula kwa ajili ya mifugo yake anatakiwa kusimamia kiwango cha wanga (mahindi/mtama) kama msingi wa vipimo vingine. Wafugaji wengine wanatumia kipimo cha ‘gunia la pumba’ kama kigezo cha kujua atahitajika aweke mahindi au dagaa kiasi gani, hiyo sio sawa. Kipimo cha ‘mahindi’ ndio kiwe kigezo cha kupata vipimo vingine, kwa sababu ‘wanga/starch’ ndio yenye sehemu kubwa ya ujazo wa kila aina ya chakula cha kuku. Ongezeko la pumba halipelekei ongezeko la utagaji mayai, bali ni ujazo tu wa makapi ya mlo (fibres).


Endelea kututembelea  [Sayuni Poultry Gosheni] ili ujifunze makala zaidi kuhusu mchanganuo wa utengenezaji wa chakula cha kuku. Tunaamini kuwa itakuwa rahisi kwako mfugaji kujifunza  mchanganuo wa utengenezaji chakula (feeds formula) pale utakapokuwa umejiridhisha kwanza katika ujuzi wa chakula bora (starch, protein, vitamins & fat contents).

Tunakushauri utumie vema eneo la kiwanja chako na ‘nguvu kazi ya nyumbani kwako’ (house-maids au vijana walio likizo za shule au wasio na kazi rasmi) katika kuzalisha kipato zaidi kupitia UFUGAJI na sio kuzalisha gharama.[ Effective use of area and human labour as an ASSET ]


Sayuni Poultry Gosheni | 0712 057 714 na 0754 282 869 | poultrysayuni@gmail.com| Mbezi Mwisho



[Part 1 MABANDA] MAMBO 4 MUHIMU YA KUKUFANIKISHA KATIKA UFUGAJI KUKU.

Mambo 4 muhimu ya kukufanikisha katika ufugaji kuku. [Part 1]

Kuweza kufanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, mfugaji  anahitaji muongozo mzuri na umakini katika MABANDA, CHAKULA BORA, UDHIBITI WA MAGONJWA na MASOKO.

Ni muhimu sana kwa mfugaji  kujifunza mambo kadhaa kabla ya kuingia kwenye ufugaji. Ni wajibu wetu [Sayuni Poultry Gosheni] kukushirikisha ufahamu huu, ili mfugaji binafsi awe muangalizi mkuu wa mradi wake; na awe na mapenzi kwa mifugo na ufugaji (tender loving care), sambamba na kuweza kuona fursa za masoko.

Baadhi ya wafugaji  hutazamia kujipatia kipato kikubwa kutoka kwenye mifugo, lakini wameshindwa kuwekeza katika mifugo hiyo ili kuweza kuzalisha kipato hicho. Lazima mfugaji makini ajifunze jinsi ya kuitunza mifugo iweze kumzalishia faida kwa kiwango cha juu.

Ingawa ‘masoko’ ndio jambo la msingi, lakini ‘udhiditi wa magonjwa’, ‘ubora wa chakula’ na ‘mabanda bora’; yote hayo yana umuhimu wake katika ufanisi wa ufugaji.

MABANDA  (housing)

Uhifadhi wa mifugo una changamoto zake kwa mfugaji wa kuku haswa katika ujenzi wa mabanda. Hapa tunaongelea ‘ufugaji huria’ kwa ajili ya kutaga mayai na nyama. Kwa dhana hiyo, mabanda ni lazima yaweze kuhifadhi mifugo dhidi ya baridi kali, upepo mkali na joto kali. Pia ulinzi dhidi ya mbwa, paka pori, panya, nyoka au vicheche ni lazima uzingatiwe. Mabanda yajengwe kwa kutazama upande wa Mashariki, ili kuisaidia mifugo kupata kivuli cha kutosha wakati jua linaelekea upande wa Magharibi. Jua kali au joto kali si zuri sana kwa mifugo hivyo mfugaji anawajibika kuwatengenezea mazingira rafiki yenye kivuli wastani.

Eneo la mita ya mraba MOJA linatosha kwa idadi ya kuku wanaotaga watatu (3) hivyo mfugaji ahakikishe kuna eneo la kutosha ili kupunguza msongamano, unaoweza kusababisha ubabe, kudonoana, ‘stress’ na hata magonjwa. Pia mifugo wanahitaji eneo la wazi nje ya banda kwa ajili ya mapumziko na kustarehe (chicken run area) ili kujipatia hewa safi, kula vijidudu na majani. Eneo la nje ni muhimu sana kwa majogoo kuonyesha umahiri wao. 




Hakikisha viota vya kutagia mayai vinawekwa eneo lisilo na mwanga/ eneo lenye kiziga ili kuku wanaotaga wasionekane kwa uwazi (respect their privacy) na pia kuwa mbali na kuku wengine wataoweza kuwabughudhi wakati wa utagaji. Mfugaji aweke ‘maranda ya mbao’ ndani ya banda na eneo la kutagia, na kuhakikisha hali ya ukavu inadumu ndani ya banda . Zingatia usafi ufanyike kila baada ya siku 4 au 5 ili kuzuia banda kuwa na unyevu, ambao unaweza kupelekea mlipuko wa magonjwa na maambukizi. Upuliziaji wa dawa za kuua wadudu mara kwa mara (spraying of disinfectants) utaongeza tija katika usafi ili kudhibiti vijidudu viambukizavyo magonjwa ndani ya banda. Pia uzingatie yafuatayo;

1. Tumia eneo la ardhi lenye mwanga na kivuli cha wastani kwa ajili ya kujenga banda la mifugo. Eneo live kavu, lenye mawe mawe, ila lisiwe eneo linaloweka maji yanayotuama, tope au eneo linalopitisha maji/ mkondo wa maji wakati wa mvua. Zingatia kuwatenga kuku wanaotaga mayai na wale wanaofugwa kwa kusudi la nyama.

2. Hakikisha upatikanaji wa uhakika wa maji, umeme, chakula na huduma za afya ya mifugo ili kuwa na mazingira rafiki yenye kukidhi mahitaji ya ziada ya mifugo na afya zao.

3. Zingajia kujifunza hadi kupata uzoefu wa kutosha katika ufugaji, kwani kwa kufanya hivyo utaweza kuwa msimamizi mkuu uliyejiridhisha katika shughuli nzima ya ufugaji. Kinyume chake itakuwa rahisi kwa wasaidizi wasio waaminifu kukupa taarifa zisizo sahihi kuhusiana na afya, maendeleo na utagaji wa mifugo yako. Hivyo inakulazimu kutenga muda wa usimamizi makini kwa matendo na sio kwa kupokea taarifa tu.

4. Hakikisha paa la banda lipo imara, kwani uvujifu wa paa utapelekea maji kupenyeza ndani ya banda; na pia hakikisha sakafu nayo ipo imara ili kuzuia maficho ya wadudu kama utitiri, papasi, chawa na maficho ya panya. Mapungufu yeyote ni hatari kwa utunzaji na afya ya mifugo wako. Ikiwa eneo la nje ya banda halina hifadhi ya kivuli, hakikisha unafanya ubunifu wa kuwepo kivuli.

5. Banda linatakiwa kupitisha hewa ya kutosha wakati wote. Urefu wa tofali 3 kutoka kwenye sakafu unafaa zaidi, na paa lichomoze kama futi 3 au 4 zaidi ya usawa wa ukuta ili maji ya mvua yasipate nafasi kupenyeza ndani ya banda kupitia dirishani.

6. Upatikanaji wa mwanga (lighting) ni jambo la kuzingatiwa pia haswa kwa vifaranga, na kuku wanaokua na kuku wanaotaga. Kwani mwezi Julai [ 15 July 2016 ] kuchomoza kwa jua ni saa 12:36 asubuhi; wakati mwezi November [15 Nov 2016] kuchomoza kwa jua ni saa 11:55 asubuhi. Mwezi Januari [ 15 Jan 2016 ] kuzama kwa jua ni saa 12:47 jioni; wakati mwezi Mei [ 15 May 2016 ] kuzama kwa jua ni saa 12:13 jioni.


Hii inamaanisha kuwa kuku wapewe chakula mapema kabla jua halijakuwa kali kwani jua kali/ joto kali litawaathiri. Wakati mwingine nuru ya asubuhi huchelewa kuangaza, haswa miezi ya Februari hadi Julai na Agosti. Hivyo ni muhimu kuratibisha upatikanaji wa mwanga kwaa kusudi la kuipatia mifugo muda wa kutosha wa chakula.

7. Usafi wa banda ni jambo la kuzingatiwa sana, sana, sana ( soma zaidi kwenye Part 3 ya muendelezo wa somo letu ) Hakikisha ‘samadi’/kinyesi chote kinazolewa na kuwekwa mbali na mifugo, kwani inzi wachafu ni wasambazaji wa magonjwa ya mfumo wa tumbo. Ukiweza kuwa na ‘spraying pump’ pamoja na ‘disinfecants’ na kupulizia kwenye mabanda , itaongeza tija sana kuliko usafi wa kawaida tu. Epuka usafi wa kutimua vumbi kwani utalipua ugonjwa wa mafua.

8. Ikiwa unafuga kwa kutumia ‘cages’ ambao ni mfumo wa kudhibiti kinyesi kuwa mbali na kuku, unashauriwa kuwa na utaratibu wa mara kwa mara kunyunyizia majivu au chokaa, na pia kuuondoa uchafu huo, kwa maana uvundo wake utaathiri mzunguko wa hewa na afya ya mifugo kwa ujumla.

9. Ndani mwa banda kubwa, unaweza kuwa mbunifu kujenga vyumba (partition) kwa ajili ya kuwatenga kuku wagonjwa, au majogoo ya hifadhi ‘reserve’, au kuwaweka lock-up matetea usiotaka waatamie kwa wakati huo.

10. Ikiwa unafuga mifugo mingineyo mfano khanga au bata mzinga, tunashauri uiweke katika uhuru wao binafsi ili kujenga utulivu katika utagaji. Kamwe usichanganye au kufuga bata maji karibu na mifugo mingine, kwani maambukizi ya ugonjwa wa typhoid yatakuwa makubwa yakiambatana na hasara kubwa au hata kufa kwa mradi wa ufugaji kuku.

HAYA ndio tumeweza kujifunza leo kwa uchache. Usikose kusoma PART 2 ya muendelezo wa elimu hii ya ufugaji kuku inayoletwa kwako na kwetu.


Sayuni Poultry Gosheni | 0712 057 714 na 0754 282869 | poultrysayuni@gmail.com| Mbezi Mwisho